Funzo Uswahiba wa Mkapa, JPM

ninamjengea Mkapa, ndiyo ninamjengea kwa sababu bila Mkapa mimi nisingekuwa waziri, inawezekana pia Urais msingeniona, sasa kumjengea barabara tu hata siku akienda kwao apite kwenye lami ni kosa? Najua Mkapa amenitoa wapi,” hii ni sehemu ya hotuba ya Rais Dk John Magufuli ‘JPM’ aliyoitoa Aprili 4, mwaka huu wakati akiwa ziarani mkoani Mtwara.

JPM aliongeza; “Watasema namjengea Mkapa barabara, nafahamu Mkapa amenitoa wapi, ndiyo ninamjengea, mwenye kununa na anune.”
Kauli hiyo ya Rais Magufuli pamoja na nyingine kadhaa alizozitoa, zimeendelea kudhihirisha ukaribu wake na Rais Mstaafu Benjamin Mkapa ulivyosheheni safari ya kipekee na funzo kwa wengi.

Safari yao ambayo imeegemea kwenye maisha ya kisiasa, pia inashabihiana na historia ya ukuaji kisiasa kati ya Mkapa alivyokuzwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julus Kambarage Nyerere.
Kutokana na hali hiyo, imeelezwa kuwa ni funzo kwa wanasiasa na viongozi mbalimbali nchini ambao hutumia vema nafasi walizopatiwa kujijenga kisisasa na kiuongozi.

SAFARI YA KISIASA
Uswahiba wa Mkapa na Magufuli ulikolea kuanzia mwaka 1995, baada ya Magufuli kuacha kazi katika Kiwanda cha Nyanza Cooperative Union akiwa Mkemia na kuwania ubunge kwa mara ya kwanza mwaka 1995.
Wote kwa pamoja walikuwa wakiwania nafasi zao kwa mara ya kwanza ambapo Mkapa alikuwa akiwania kiti cha Urais ilihali Magufuli aliwania ubunge Jimbo la Biharamulo Mashariki (kwa sasa ni Chato).
Hali hiyo ilichangia Mkapa kumnadi kindakindaki Magufuli ambaye alikuwa mchanga kwenye siasa na akafanikiwa kunyakua jimbo hilo.

Baada ya Magufuli kushinda ubunge na Mkapa kushinda kwa kishindo Urais, Magufuli aliteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Miundombinu.
Katika uchaguzi wa mwaka wa 2000 pia aligombea ubunge na kushinda na Rais Mkapa akamteua kuwa Waziri wa Miundombinu.

Katika uchaguzi wa mwaka 2005 Magufuli aligombea ubunge kwa mara ya tatu na kupita bila kupingwa na Rais Jakaya Kikwete hakumwacha katika baraza lake la mawaziri kwani alimteua kuongoza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na baadaye Wizara ya Mifugo na Uvuvi.

Hata hivyo, 2010 alichaguliwa kuwa mbunge kwa mara ya nne na Rais Kikwete alimrudisha katika Wizara ya Miundombinu na Ujenzi ambako alidumu hadi alipogombea urais mwaka 2015.
Teuzi hizo zote zilidhihirisha namna Mkapa anavyomkubali Magufuli na kusema kuwa ni askari mwamvuli namba moja katika baraza lake la mawaziri.
Vivyo hivyo kwa upande wa Rais Kikwete alisema Magufuli ni ‘buldoza’ kwa mantiki kuwa kila mahali linapita na kusafisha njia.

URAIS
Katika safari ya urais, Magufuli mara kadhaa baada ya kunyakua kiti hicho amekuwa hafichi furaha yake namna alivyopikwa na Mkapa.
Furaha hiyo ya Magufuli inatokana na ukweli kwamba katika kinyang’anyiro cha urais mwaka 2015, imeelezwa kuwa Mkapa ndiye aliyezima vurugu katika kikao cha Halmashauri ya CCM (NEC) baada ya wajumbe wake kuimba wana imani na Edward Lowassa.

Kikao hicho kilichofanyika Julai 10, 2015 kilionekana kuelekea kukumbwa na mtafaruku baada ya wajumbe kumpokea Rais Kikwete kwa wimbo wa kuonesha wana imani na waziri huyo mkuu wa zamani ambaye jina lake halikuwamo miongoni mwa makada watano waliopitishwa na Kamati Kuu ya CCM.
Mkapa ambaye alikuwa mjumbe wa baraza la wazee la ushauri CCM, aliwaambia wajumbe hao kupiga kura na wale wasioafiki watoke nje.

CHANGAMOTO
Kila jambo lina changamoto na ndivyo ilivyotokea kwa uswahiba huo wa Magufuli na Mkapa ambapo almanusura uingie doa baada ya Magufuli kutaka kujiuzulu uwaziri katika kipindi hicho cha uongozi wa Mkapa.
Hayo yalidhihirishwa na Magufuli baada ya hivi karibuni kukiri kuwa sifa alizopatiwa na Mkapa kutokana na utendaji wake zilisababisha apewe sumu.

“Siwezi kusahau suala hilo maishani mwangu kwa kuwa liliniletea matatizo, nilianza kuona dalili za baadhi ya mawaziri tena wengine wa ngazi za juu kuanza kunichukia,” alisema Magufuli.
Alisema baada ya kunusurika kifo alimfuata Mkapa kumweleza dhamira yake ya kutaka kujizulu.
“Nakumbuka siku hiyo aliniangalia jicho la baba na mwana akanihurumia, alinipa ujasiri akaniambia John kafanye kazi, kamtangulize Mungu.”

Hata hivyo, itakumbukwa kuwa Mei, mwaka huu, Rais Magufuli alimteua Mkapa kuwa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) ambacho hivi karibuni kilifanya mahafali ya 10.
Katika mafahali hayo, Rais Magufuli alibainisha changamoto nyingine aliyoipata kutoka kwa Mkapa baada ya kumpatia barua ya kutaka kumtunuku shahada ya heshima ya udaktari wa falsafa.

“Napenda nikiri Mkapa atakumbuka, baada ya kupewa barua, nilikaa mwezi mzima sijajibu, wasaidizi wangu wakanikumbusha kuwa sijajibu barua, nikawaambia nitajibu, dhamira yangu ilikuwa inanisuta kwa nini nipewe cha bure, ile ‘knowledge’ ya baba ilikuwa inanisuta, lakini nikakumbuka historia yangu na mzee Mkapa,” alisema.

UCHAPAKAZI
Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Ruaha, Profesa Gaudence Mpangala alisema uchapakazi wa Magufuli ulimfanya walio juu yake, (Mkapa na Kikwete) kuendelea kumwamini na kumpa nafasi.
Alisema utendaji wake ni moja ya mambo yaliyomfanya Mkapa kumuona na kumuendeleza kisiasa hadi aliponyakua urais.

Post a Comment

0 Comments