Ifahamu historia ya mchezaji Fernando Torres


Desemba 29, 2009 nyota wa kandanda wa klabu ya Liverpool wakati huo na timu ya taifa ya Hispania Fernando Torres maarufu El Niño alifunga bao lake la 50 la ligi kuu akiwa na Liverpool.

Torres alifunga bao hilo la  50 katika Ligi Kuu tangu alipotua katika hiyo klabu ya Liverpool na kuweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza kuifikia rekodi hiyo kwa haraka kwenye historia ya miamba hiyo ya Anfield.


Aidha bao hilo lilikuwa la 52 katika mashindano yote tangu alipotua Anfield. Torres alitua Liverpool akitokea Atletico Madrid ya Hispania mnamo Julai 2007 wakati huo akiwa na miaka 23.

Mechi yake ya kwanza katika Ligi Kuu ya England ilikuwa Agosti 11, 2007 ambapo alifunga bao lake la kwanza katika sare ya 1-1 na Chelsea.

Katika mwaka wake wa kwanza katika ardhi ya England Torres alifunga mabao 33 akiisaidia Liverpool kushika nafasi ya nne katika msimamo wa Ligi Kuu nchini England.

Pia alifanikiwa kuifikisha nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa barani Ulaya.  Katika msimu huo mabao 24 aliyafunga katika Ligi Kuu.

Majeruhi yalimfanya katika msimu wake wa pili pale Merseyside asing’are kama msimu wake wa kwanza kwani alifunga mabao 14 tu. Katika mapambano hayo aliisaidia Liverpool kumaliza nafasi ya pili ya msimamo wa Ligi Kuu.

Rekodi ya kufunga bao la 50 tangu alipokanyaga England ilifikiwa katika msimu wake wa tatu katika mchezo dhidi ya Aston Villa.

Katika dakika za majeruhi  bila timu kuliona lango la mwenzake Torres alimalizia rebound na kumshinda mlinda mlango Brad Friedel na kuipa ushindi Liverpool.

Bao hilo alifunga ikiwa ni mechi yake ya 72 akiwa na Majogoo wa Anfield, akiipita rekodi ya mkali mwingine wa Liverpool Sam Raybould aliyeitumikia Liverpool mwaka 1900-1907 akifunga mabao 120 katika mechi 211. Sam alifunga mabao 50 baada ya mechi 80.

Pia Torres alimpita mfungaji wa zama zote wa Liverpool Ian Rush aliyeitumikia miamba hiyo kwa vipindi viwili tofauti mnamo mwaka 1980-1987 na 1988-1996 akifunga mabao 346. Hata hivyo Rush alifunga mabao 50 akiwa na Liverpool baada ya mechi 84.


Torres alizaliwa Machi 20, 1984 akianza maisha yake ya soka katika akademi ya vijana ya Atletico Madrid na baadaye timu ya wakubwa. Akiwa nchni Hispania alifunga mabao 75 katika mechi 174 za La Liga.

Wakati anatua Liverpool mnamo mwaka 2007 aliweka rekodi ya kwanza ya kufunga mabao zaidi ya 20 baada ya Robbie Fowler aliyefanya hivyo msimu wa 1995-96.


Januari 2011 aliachana na Liverpool na kujiunga na Chelsea kwa rekodi ya Pauni milioni 50 ikiwa ni uhamisho ghali zaidi katika historia ya soka la England wakati huo kwa mchezaji kutoka Hispania.

Post a Comment

0 Comments