Morrison Ashusha Presha, Atoa Kauli ya Kibabe Yanga SC

Mghana Bernard Morrison.
KIUNGO mshambuliaji fundi wa Yanga, Mghana Bernard Morrison amewaondoa hofu mashabiki wa timu hiyo kwa kuwaambia kuwa amepata nafuu ya majeraha yake, hivyo atakuwa sehemu ya wachezaji watakaoivaa Namungo FC.

Yanga kesho inatarajiwa kujitupa kwenye Uwanja wa Majaliwa, Lindi katika mchezo wa Ligi Kuu Bara unaotarajiwa kujaa upinzani mkubwa baada ya timu hiyo kupoteza mchezo uliopita kwa bao 1-0 walipocheza na KMC juzi kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar.

Mghana huyo hakuwa kwenye sehemu ya kikosi cha timu hiyo kilichofungwa na KMC kutokana na kuuguza majeraha ya goti aliyoyapata siku tatu kabla ya mchezo wa Dabi ya Kariakoo iliyochezwa wikiendi iliyopita na Yanga kushinda bao 1-0 lililofungwa na yeye.

Akizungumza na Championi Jumamosi, Morrison alisema jana Ijumaa alimaliza siku tano alizopewa na Kocha Mkuu wa timu hiyo, Mbelgiji Luc Eymael baada ya daktari wa timu hiyo kupendekeza apumzike ili asijitoneshe jeraha lake.

Morrison alisema kuwa leo Jumamosi anatarajiwa kufanya mazoezi ya mwisho kabla ya kucheza dhidi ya Namungo baada ya juzi Alhamisi kufanya mazoezi binafsi ya kukimbia mbio fupi na ndefu.

“Niwashukuru mashabiki wote wa Yanga waliokuwa wananipa pole wakati nikiwa nje ninaendelea na matibabu baada ya kushindwa kumalizia dabi ya Yanga na Simba, nafahamu walikuwa wanatamani kuniona nikiendelea lakini majeraha yakasababisha nishindwe kuendelea.

“Nilicheza mchezo ule nikiwa nina majeraha ya goti niliyoyapata siku tatu kabla ya dabi, lakini licha ya kupata majeraha hayo nilimuomba kocha nicheze kwa kipindi kimoja, nashukuru kocha akakubali nicheze nikafanikiwa kufunga bao la ushindi.

“Tunajiandaa na mchezo dhidi ya Namungo ambao ninatarajia kuwa sehemu ya wachezaji watakaocheza mchezo huo, ni baada ya kupata nafuu baada ya kupatiwa matibabu ya haraka huku nikiwa chini ya uangalizi wa daktari, hivyo niwaondoe hofu nitakuwepo uwanjani siku hiyo wajiandae kupata furaha,” alisema Morrison.

Post a Comment

0 Comments