Umoja wa Mataifa waadhimia mambo manne, kura zapigwa kwa njia ya Barua pepe hofu ya CoronaBaraza la usalama la Umoja wa Mataifa kwa kauli moja limeidhinisha maazimio manne hapo jana siku ya Jumatatu, wakati wajumbe wake 15 wakipiga kura kwa kutumia Barua pepe kwa mara ya kwanza kutokana na janga la Virusi vya Corona.
Wajumbe wamepiga kura ujumbe wake wa kulinda amani kuendelea kuwapo katika jimbo la Darfur hadi mwishoni mwa Mei na kuendeleza ujumbe wa kisiasa wa Umoja wa mataifa nchini Somalia hadi Juni 30.
Wamerefusha muda wa jopo la wataalamu wa Umoja wa Mataifa wanaoangalia utekelezwaji wa vikwazo dhidi ya Korea Kaskazini hadi Aprili 30, 2021, na wamesisitiza umuhimu wa kuunga mkono operesheni za Umoja wa Mataifa za kulinda amani katika maeneo mbali mbali duniani.
Chombo hicho muhimu cha Umoja wa mataifa kimekuwa kikifanya mikutano kwa njia ya Video kwa sababu ya ugonjwa wa COVID-19, ambao umeukumba mjini New York , ambako Umoja wa Mataifa una makao yake makuu.

Post a Comment

0 Comments