Chuji avunja rasmi mkataba na SingidaKIUNGO mkongwe nchini, Athumani Idd 'Chuji', amesema amevunja mkataba wake na klabu yake ya Singida United kwa sababu hawakumpa mshahara wa miezi mitatu.


Akizungumza jijini Dar es Salaam, Chuji alisema kwa sasa si mchezaji wa Singida United kwa sababu wamevunja makubaliano, kwani kwenye kipengele cha mkataba alisaini kuwa asipolipwa mshahara wa miezi miwili basi mkataba wake umevunjika.

"Kwa sasa niko huru kwa sababu nilisajiliwa kumalizia ligi kipindi cha dirisha dogo, lakini hadi naondoka nilikuwa sijalipwa miezi mitatu," alisema Chuji ambaye ni mmoja wa wachezaji wachache waliowahi kuzichezea klabu kubwa nchini za Simba, Yanga na Azam FC.

Kwa maana hiy,o kiungo huyo mkabaji, aliyekuwa akisifika kwa mashuti makali na pasi ndefu za uhakika, amejiweka sokoni ili timu yoyote inayomtaka ifanye mawasiliano naye.

Kuhusu klabu ya Singida United, Chuji alisema, anayejitahidi kwa sasa kuhakikisha haishuki na kuendelea kucheza ligi ni Waziri wa zamani wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba, ambaye anaonekana yupo karibuni na timu, huku baadhi ya viongozi wakionekana kama kuisusa.

"Nashangaa watu wa Singida siyo kama wa Mtwara ambako Ndanda FC kila mwaka inapokuwa kwenye hali mbaya, basi wanakwenda kwa viongozi wa mkoa kama vile Mkuu wa Mkoa na viongozi wengine wa kisiasa kuhamasisha wananchi timu kuwa haishuki na wanafanikiwa sana kwa hilo, Ndanda huwa inasalimika kwa kubakia Ligi Kuu, nashangaa kwa nini watu Singida hawafanyi hivyo." alisema.

Chuji pia aliwalaumu baadhi ya watu ndani ya klabu hiyo kutaka ishuke kwa maslahi yao, halafu waipandishe.

"Mimi nishawasikia kuna watu wanasema wanataka timu ishuke, halafu wao wataipandisha, sasa hawa wanaitakia mema klabu au wana maslahi yao?" alihoji.

Post a Comment

0 Comments