Paul Kagame: Hakuna wanajeshi wa Rwanda walioingia DRC

Rais wa Rwanda Paul Kagame amekanusha madai kuwa wanajeshi wa nchi yake walivuka mpaka hivi karibuni na kuingia nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kupambana na makundi ya waasi.
Kagame amesema hakuna hata mwanajeshi mmoja wa RDF katika eneo la Mashariki mwa nchi hiyo kama ambavyo mashirika ya kiraia na wanasiasa wa upinzani nchini DRC wamekuwa wakidai.
Hivi karibuni mashirika ya kiraia mkoani Kivu kaskazini nchini DRC yalilaani kitendo cha wanajeshi wa Rwanda kuingia nchini humo na kutekeleza operesheni ya kuyasaka makundi ya waasi wa Rwanda katika eneo la Nyiragongo mbali kidogo na mji wa Goma.
Kwa Mujibu wa mashirika hayo ya kiraia eneo la Nyiragongo, hakuna anayeweza kukanusha hili, kwamba wanajeshi wa jeshi la Rwanda walivuka mpaka wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na kubaini kuongezeka kwa matukio yanayowasababishia wakaazi wa eneo hilo kuishi wakiwa na wasiwasi mkubwa, huku miongoni mwa matukio yaliyotajwa ni pamoja na mwanajeshi mmoja wa Rwanda kujeruhiwa kwa risasi katika eneo la Kabara, karibu na uwanja wa kimataifa wa ndege wa Goma mwanzoni mwa mwezi Aprili mwaka huu.
Sio mara ya kwanza Rwanda kushtumliwa kuingiza askari wake katika ardhi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kuyasaka makundi ya waasi wa Rwanda yanayopiga kambi Mashariki mwa nchi hiyo.Post a Comment

0 Comments