Uchaguzi wa Tanzania 2020: Je, muungano wa UKAWA kurudi tena?

Kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka minne Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimeshiriki sherehe ya kitaifa ya maadhimisho ya miaka 58 uhuru wa Tanganyika mnamo Disemba 9 mwaka huu iliyofanyika kwenye uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.
Freeman Mbowe, Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni na mwenyekiti wa Chadema aliwaongoza vigogo kutoka chama chake kushiriki sherehe hizo, Godbless Lema (Mbunge wa Arusha), Joseph Mbilinyi (Mbunge wa Mbeya Mjini), Lazaro Nyalandu (Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kati), John Mnyika (Mbunge wa Kibamba), Boniface Jacob (Meya wa Ubungo), na John Heche (Mbunge wa Tarime).
Wanasiasa hao kwa kauli moja wanaonekana kukubali sasa ni zama za maridhiano ya kisiasa ili kile kinachoitwa 'kuponya' taifa hilo ambalo lilishuhudia vyama vya upinzani vikijitoa kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa.
Aidha, Chadema wameshuhudia vigogo wa chama hicho wakifunguliwa mashtaka mahakamani, kukosa vibali vya mikutano ya hadhara, wimbi la wabunge kuhamia CCM ni miongoni mwa mambo yaliyokoka moto wa siasa.
Uamuzi wa Chadema umeibua mjadala kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 kuhusu nafasi ya muungano wa Umoja wa Katiba ya wananchi maarufu kwa jina la UKAWA.
Sumaye: Chama cha Chadema hakina demokrasia.
Vyama vya upinzani vilipojitoa kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka huu vyote vilitoa kauli moja yenye lengo la kutuma ujumbe kwa mamlaka za Tanzania kuwa hali ilikuwa mbaya kisiasa. Kauli hiyo iliwaimarisha upinzani.
Duru za kisiasa zinahoji ni namna gani Chadema wanaweza kusimamia muungano wa upinzani wa UKAWA ambao uliwezesha kupatikana kura milioni 6 za urais na viti vingi vya bunge kuliko wakati wowote katika historia ya vyama vya upinzani nchini.

Hekaheka za Ukuta

Kudhihirisha demokrasia inasiginwa nchini Tanzania, mwaka 2016 Chadema kwa kushirikiana na vyama vingine vya upinzani waliandaa maandamano yaliyoitwa jina la Ukuta, kwa maana ya Umoja wa Kupambana na Udikteta Tanzania, ambayo yaliahirishwa siku moja kabla ya kufanyika Septemba mosi.
Katika kipindi hicho viongozi hao walitoa sababu ya kuahirisha zilitokana na maombi ya viongozi wa kidini waliopendekeza kutangulizwa mazungumzo baina ya upinzani na serikali.

Je, upinzani kudumisha mshikamano?

Mshikamano miongoni mwa vyama vya siasa vya upinzani unakiamsha chama tawala CCM kukuza demokrasia,kuleta maendeleo, kudumisha utawala bora, na haki za binadamu.
Wakati Rais Magufuli na Chadema wanakaa meza moja, mwanasiasa Tundu Lissu wa Chadema na kiongozi wa chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe katika nyakati tofauti wametangaza nia ya kugombea urais 2020, hali ambayo ikakoka joto la uchaguzi huo mkuu juu ya uamuzi gani unachukuliwa na upinzani katika kuteua mgombea wao.
Zitto Kabwe na Freeman MboweHaki miliki ya pichaCHADEMA,TWITTER
Image captionJe, upinzani kudumisha mshikamano?
Mwanasheria na mchambuzi wa masuala ya siasa na utawala bora, Jovinson Kagirwa amemwambia mwandishi, "Ni vigumu kufanya siasa za kirafiki na watu wanaofanya siasa za mabavu. Siasa inayoendana nao ni siasa ya harakati. Sasa harakati inahitaji mshikamano wa makundi ya kiraia na vyama vya upinzani.
Ameongeza, "Lakini vyama vya upinzani kwa sasa haviwezi kuwa na umoja wa aina yoyote ile katika siasa hizi za 2015-2020. Sababu kubwa ni kwamba hakuna tena kitu kinachowaunganisha kama ilivyokuwa mwaka 2014 wakati wanaungana.
UKAWA ulianzishwa mwezi Oktoba 2014 kulikuwa na kitu kilichowaunganisha vyama vya siasa za upinzani ambacho ilikuwa ni katiba mpya, kama ilivyokuwa katika rasimu ya Tume ya katiba dhidi ya mapendekezo au msimamo wa chama tawala na serikali kwa ujumla.
"Kwa maana hiyo kutokana na mvutano ule uliokuwepo ilionekana wazi kuwa njia pekee ya wapinzani kushinda ni kurudi kwa wananchi ambao ndio wangeamua ni katiba ipi itumike katika kura ya maoni ya katiba. Ilikuwa njia ya kuunganisha nguvu kuweza kuungana na wananchi dhidi ya chama tawala na serikali.
Dk. Wilbroad Slaa akiwa Katibu mkuu kipindi hicho alisema kuwa lengo kubwa ni kuhusisha sera za vyama vyote na kuchukua yale yanayofanana ili wawe na kauli zinazolingana. Huu ulikuwa umoja unaotumia suala la katiba kuweza kupata nguvu na kuungwa mkono na wananchi,"

Je Chadema wanamwimarisha Rais Magufuli?

Uamuzi wa sasa Chadema kushiriki sherehe za uhuru na wanasiasa wa chama hicho kusisitiza maridhiano, kutachochea mshikamano wa upinzani au ni mwanzo wa mwisho wa UKAWA?
Ado Shaibu, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa ACT-Wazalendo amemwambia mwandishi kuwa chama chao hakina mamlaka ya kuwazuia Chadema, licha ya hatua yao kuonyesha inampigia kampeni Rais Magufuli, lakini wapo tayari kushirikiana nao kwenye masuala mengine ya siasa za upinzani nchini Tanzania.
"Mimi nina imani kila chama kina uhuru wa kuchagua mkondo wa kufuata. Wakati wenzetu wanaamini kushiriki sherehe za Uhuru ilikuwa ni ishara ya kufungua milango ya maridhiano, sisi tuna imani kuwa hatua hiyo inamuimarisha zaidi Rais Magufuli. Licha ya tofauti zetu kimsimamo, nina imani kuwa ushirikiano kwenye masuala mengine ya kitaifa kama vile kupigania demokrasia na kushirikiana kwenye uchaguzi zitaendelea," amesema Ado Shaibu.

Je, kuna kambi mbili upinzani?

Viongozi wa ChademaHaki miliki ya pichaHISANI
Image captionJe, kuna kambi mbili upinzani?
Watia nia ya urais Tundu Lissu na Zitto Kabwe wana ushawishi katika kambi ya upinzani. Vyama vyao vinahitajiana, lakini duru za kisiasa zinasema zipo pande mbili zinazosigina waziwazi ambazo huenda zikashindwa kufanya kazi pamoja.
Richard Ngaya, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Sokoine na mchambuzi wa siasa na utawala bora, amemwambia mwandishi wa makala haya, "Siioni UKAWA ya mwaka 2015 katika uchaguzi mkuu ujao, hasa kwa kuzingatia historia ya Zitto Kabwe na Chadema na wakati huu ambapo ni kiongozi mkuu wa chama cha ACT-Wazalendo kilichochukua mtaji wa zamani wa chama cha CUF visiwani Zanzibar.
Tundu Lissu
Image captionMwanasiasa maarufu wa Tanzania kupitia CHADEMA, Tundu Lissu
Amesisitiza kuwa, "Zitto mara kadhaa ameeleza wazi kutamani nafasi ya kuwa rais wa nchi na kwa namna moja unaweza kusema yuko tayari kugombea urais mwaka 2020.
Je Chadema wanaweza kukubali kuungana na ACT-Wazalendo ya Zitto Kabwe na kumpa nafasi hiyo? Na wakitokea kuungana halafu wasimpe nafasi ya kugombea atakuwa tayari kutumia chama chake kupata ushindi kwa niaba ya Muungano huo kule Visiwani Zanzibar au atajiondoa?
"Hapo ndipo pagumu kwa muungano wa vyama vya upinzani kwenye uchaguzi wa 2020. Lakini pia mazingira ya siasa za sasa kuelekea uchaguzi mkuu mwakani hayaonekani kuruhusu ushindani ulio huru kwa maana mtu kushinda kwa sababu ya sanduku la kura.
Kuna dalili zote kuwa watu wa upinzani wana nafasi finyu ya kufanya siasa sawa na chama tawala hasa tukizingatia mwenendo wa vyombo vya dola pamoja na watumishi wa umma kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa na kabla ya hapo.
Hayo yote yanainyima nafasi UKAWA kuundwa na kuingia kwenye ushindani wa kweli mwakani.
"Naona vyama binafsi vikisimama kila chama peke yake ama kuunda kambi mbili, moja ikiwa na Chadema na nyingine ya ACT-Wazalendo kama kiongozi huku chama tawala CCM kikipita kiurahisi hata bila kutumia nguvu ya vyombo vya dola.

Post a Comment

0 Comments