Wabunge 17 wahofiwa kuwa na corona Kenya

 Wabunge 17 kati ya 50 wa Kenya wanahofiwa kuambukizwa virusi vya corona vinavyosababisha ugonjwa wa Covid-19.

Hata hivyo, Spika wa Bunge la Kenya, Justin Muturi amesema kuwa habari hizo si za kweli kwa kuwa kila mbunge alipewa majibu yake baada ya kuchukuliwa vipimo.

Wiki iliyopita wabunge 50 walichukuliwa vipimo kwa hiari ili kubaini iwapo wameambukizwa ugonjwa huo ambako majibu yalibaki kuwa siri ya mgonjwa na daktari.

Kufuatia sintofahamu hiyo, Spika Muturi ametangaza kuahirisha mkutano wa Bunge hilo uliokuwa uanze vikao vyake Jumanne ya Aprili 7.

Kwa mujibu wa Gazeti la The Daily Nation la Kenya, kuahirishwa kwa vikao hivyo kunatokana na onyo la Wizara ya Afya kuonya kuwa hakutakuwa na maana ya kuendelea na vikao bila kujua majibu ya jumla ya wabunge wote waliopimwa.

Vyanzo mbalimbali vya habari vililieleza gazeti hilo kuwa wabunge 17 walithibitika kuwa na maambukizi hayo.

Hata hivyo, taarifa ya wabunge hao haikutolewa jana na waziri huyo katika utaratibu wake wa kuhabarisha umma kila siku badala yake alisema kuna maambukizi mapya 14.

Karani wa Bunge, Michael Sialai alisema hana taarifa kamili kuhusiana na maambukizi hayo.

“Vipimo vilikuwa vya hiari na majibu yalikuwa kila mmoja anapewa ya kwake,” alisema Sialai.

Kupitia ujumbe wa simu uliotumwa Jumatatu iliyopita uliwataarifu wabunge wote kuwa Bunge limeahirishwa ili kuchunguza afya na usalama wa viongozi hao pamoja na wafanyakazi wa taasisi hiyo.

Hadi jana jioni nchi hiyo ilikuwa na wagonjwa wa virusi vya corona 179 na sita kati yao walifariki dunia.

Vikao vya Bunge hilo vinavyokutana Jijini Nairobi vilitarajiwa kuanza leo.

Kauli ya Spika wa Bunge

Akizungumza na waandishi wa habari, Spika Muturi alisema kikao hicho kilifutwa baada ya Rais Uhuru Kenyatta kuweka marufuku ya kutosafiri nje na kuingia Jijini Nairobi.

Alisema masharti hayo ya usafiri yanalenga kuzuia kuenea kwa virusi vya corona hivyo Bunge haliwezi kupingana na amri hiyo. Mji wa Nairobi na Pwani ya Mombasa imetajwa kuwa maeneo hatari kwa kasi ya maambukizi ya virusi vya corona.

Post a Comment

0 Comments