Balozi Agustine Mahiga na safari ya utumishi wa miaka 45 kwa Tanzania na UN


Augustine Philip Mahiga, ambaye amefariki hii leo jijini Dodoma ni moja ya wanadiplomasia mahiri kuwahi kutokea nchini Tanzania.
Pia ni moja kati ya watu wachache amabao wamefanya kazi katika ngazi za juu na awamu zote tano za serikali ya Tanzania kutoka kwa rais wa kwanza Mwalimu Julius Kambarage Nyerere mpaka awamu hii ya rais John Pombe Magufuli.
Licha ya utajiri wake wa maarifa na uzoefu mkubwa ndani na nje ya Tanzania, Balozi Mahiga alikuwa mtu ambaye hakujikwaza kwa mamlaka yake. Na hiyo ni moja ya sifa ambayo watu wanaomuomboleza hii leo wanampamba nayo.
"Pamoja na umri wake mkubwa na uzoefu wa kushika madaraka katika nyadhifa mbalimbali za Kitaifa na Kimataifa, marehemu Balozi Mahiga alikuwa mnyenyekevu na mtiifu kwa kila jukumu nilomtuma," ameeleza Rais Magufuli katika salamu zake rasmi za rambirambi.
"Upumzike kwa Amani Balozi Mahiga. Ulikuwa mtu mwema sana," ameomboleza mbunge wa upinzani nchini humo Halima Mdee kupitia ukurasa wake wa Twitter.
Salamu za rambirambi pia zimetumwa kwa kutumia ukurasa wa Twitter kutoka balozi za Uingereza, Canada, Ufaransa, Sweden na Uchina nchini Tanzania zimemwagia sifa ya kuwa mwanadiplomasia mbobezi aliyewaikilisha vyema nchi yake.
Safari ya utumishi wa Mahiga inatoka mwaka 1975 mpaka umauti wake 2020
Image captionBalozi Mahiga, mwanadiplomasia nguli aliyehudumu kwa miongo mitano

Je, amefanya kazi gani ndani ya Tanzania?

Mpaka umauti unamfika alikuwa Waziri wa Katiba na Sheria nafasi ambayo alikuwa akihudumu toka mwezi Machi 2019.
Kabla ya hapo alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje nafasi ambayo alihudumu kutoka mwaka 2016.
Mahiga pia alikuwa mbunge wa kuteuliwa na rais mpaka umauti unamkuta.
Mwaka 2015 Mahiga alikuwa ni moja ya wananchama wa CCM ambao waligombea tiketi ya kuwania urais katika kinyang'anyiro ambacho Magufuli aliibuka na ushindi.
Mahiga pia alifundisha kama Mhadhiri Mwandamizi wa Mahusiano ya Kimataifa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam baina ya mwaka 1975 mpaka 1977.
Baada ya hapo alihamia katika ofisi ya rais Ikulu akiwa kama Mkurugenzi wa Utafiti na Mafunzo.
Kutoka mwaka 1980 mpaka 1983 akapandishwa kazi katika ofisi hiyo ya rais na kuwa Mkurugenzi wa Idara ya Usalama wa Taifa.
Pia kwa vipindi tofauti katika utumishi wake amekuwa mhadhiri mtembezi katika Chuo cha Diplomasia jijini Dar es Salaam.

Mwanadiplomasia nguli

Kwa kipindi cha miaka 30 kutoka mwaka 1983 mpaka 2013 Balozi Mahiga alifanya kazi ya diplomasia akiiwakilisha nchi yake kama balozi na pia kuwakilisha Umoja wa Mataifa (UN) katika nchi mbalimbali.
Kwa miaka sita kutoka 1983 mpaka 1989 alikuwa balozi wa Tanzania nchini Canada na kutoka 1989 mpaka 1992 akahudumu katika ubalozi wa kudumu wa Tanzania katika ofisi za UN jijini Geneva, Uswizi.
Kutoka mwaka 1992 mpaka mwaka 1994 alihudumu kama mwakilishi mkaazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Wakimbizi UNHCR nchini Liberia.
Kutoka 1994 mpaka 1998 alirudi Geneva na kuwa mratibu na mkurugenzi msaidizi wa Operesheni za Dharura za Wakimbizi katika eneo la Maziwa Makuu barani Afrika. Katika kipindi hicho kulikuwa na vita zilizoangamiza maisha ya makumi kwa maelfu ya watu na kuzalisha mamia ya wakimbizi kutoka nchi za Rwanda, Burundi na DRC.
Kutoka 1998 mpaka 2002 alikuwa mwakilishi mkaazi wa UNHCR India, na kutoka 2002 mpaka 2003 akawa mwakilishi wa Shirika hilo katika nchi za Italia, Malta na San Marino.
Mwaka 2003 akateuliwa na Rais wa awamu ya tatu wa Tanzania Benjamin Mkapa kuwa Balozi wa Tanzania katika Ofisi za Kudumu za Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa (UN) jijini New York na kusalia katika nafasi hiyo katika muhula wa kwanza wa rais wa nne wa Tanzania Jakaya Kikwete mpaka 2010.
Mwaka 2010 akateuliwa na aliyekuwa Katibu Mkuu wa UN kipindi hicho Ban Ki-moon kuwa mwakilishi wake maalum kwa Somalia nafasi ambayo alihudumu mpaka Juni 2013.
Mahiga amefariki akiwa na miaka 74 (amezaliwa Agosti 28 1945) na kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu kifo chake kimetokana na kuugua ghafla alfajiri ya Ijumaa Mei Mosi.
Alipata shahada yake ya kwanza ya Ualimu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 1970, mwaka 1971 alipata shahada ya Uzamili katika Mahusiano ya Kimataifa kutoka Chuo Kikuu cha Toronto na mwaka 1975 akahitimu shahada ya Uzamivu (PhD) ya Mahusiano ya Kimataifa katika Chuo hicho pia.
Waziri wa Katiba wa Tanzania Augustine Mahiga amefariki dunia alfajiri ya leo mjini Dodoma.
Taarifa iliyotiwa saini na Rais John Magufuli ilisema kuwa Mahiga aliugua ghafla akiwa nyumbani kwake mjini Dodoma alfajiri ya Ijumaa, Mei mosi na alifikishwa hospitali akiwa ameshafariki.

Post a Comment

0 Comments